Stori: Na Mwandishi Wetu
MACHAFUKO yanayoendelea ndani ya Baraza la Mawaziri, ni wazi yanawaweka
waheshimiwa wengi katika wakati mgumu ambapo Jumapili iliyopita, Uwazi
lilimnasa mmoja wa mawaziri (jina tunalo), kwenye nyumba ya sangoma
aliyefahamika kwa jina moja la Bwehe, Kijiji cha Mlingotini, Bagamoyo,
Pwani.
Rais Dk. Jakaya Kikwete.
Habari zinadai waziri huyo alikwenda kwa Bwehe ili kufanyiwa
madongoloji (nguvu za giza), lengo kuu likiwa kuimarisha nyota yake ili
Rais Jakaya Kikwete atakapofanya panguapangua, jina lake liendelee
kutamalaki.
Awali, Jumamosi iliyopita Uwazi lilipokea simu kutoka kwa msomaji
wetu aliyesema: “Uwazi kama kweli nyie ni gazeti la kufichua maovu,
fikeni Mlingotini kesho asubuhi mtamuona mheshimiwa … (anataja jina la
waziri) kwa mganga wa kienyeji.”
Timu ya gazeti hili ilianza safari
alfajiri ya Jumapili iliyopita na ilipotimia saa 12:50, tayari ilikuwa
imekwishawasili Mlingotini na kupiga kambi jirani na kwa Bwehe.
Hata hivyo, ugunduzi wa waandishi wetu ni kwamba wengi waliosema
hawakumuona, ni dhahiri hawamjui, kwa hiyo haikuwa rahisi kupata taarifa
zake.
Saa 3:35 asubuhi, waziri huyo alikuwa hajawasili, hivyo kuanza kuzitilia shaka taarifa za mtoa habari.
Timu ya Uwazi, ilituma taarifa makao makuu kwamba taarifa za waziri
huyo inaonekana ni feki lakini muongozo wa kuendelea kusubiri
ulifanikisha jawabu ilipotimia 3:54, pale gari aina ya Nissan X-trail
lilipowasili nyumbani kwa sangoma huyo.
Kilichotendeka ndani hakikuweza kujulikana lakini waziri huyo
alitumia takriban saa 4, kwani saa 8:07 mchana alitoka, akaingia kwenye
gari na kutoweka.
Jitihada za waandishi wetu kumuwahi ili kumuhoji sababu ya kwenda kwa
sangoma ilishindikana maana alipiga hatua kama za umeme kutoka ndani,
kuingia kwenye gari, kuwasha na kuondoka.
Mwandishi wetu
alipomtafuta waziri huyo kwa simu, alipopatikana na kuulizwa ni kwa nini
alikwenda kwa sangoma, alinyamaza kwa sekunde kadhaa kisha akazima
simu.
Bwehe alipoulizwa na mwandishi kuhusu mgeni wake ambaye ni waziri,
alikuwa mkali, akasema: “Mnataka kuingilia kazi yangu? Mnataka kujua
nguvu nilizonazo? Endeleeni kunifuatilia na mtaniona.”
Habari
zinasema kuwa tangu machafuko katika Baraza la Mawaziri yatokee, hali
imekuwa tete na wengi wao wanaoamini nguvu za giza wamekuwa
wakijielekeza kwa waganga wa kienyeji kwa imani kwamba huko ndipo
watapata nusura.
Imebainishwa kuwa wimbi la mawaziri kwenda kwa waganga, lilianza
tangu Katibu Mkuu wa CCM, Abrahman Kinana, alipozindua kampeni inayoitwa
‘safisha mawaziri mizigo’, hivyo wengi wao kukimbilia kwa sangoma kwa
imani kwamba watawezeshwa kukaa upande salama.
Bila shaka, machafuko ya Ijumaa iliyopita bungeni, yaliyofuata baada
ya kusomwa kwa ripoti ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii,
iliyoelezea athari za Operesheni Tokomeza Ujangili (Otu), yanachagiza
wenye imani dhaifu kujikita kwa waganga wakiwaona ni wakombozi wao.
Ripoti hiyo, ilisababisha mawaziri wanne, Dk. Hamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai
Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Mathayo David (Uvuvi na
Maendeleo ya Mifugo) kung’oka, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa
katika kikaango kikali.
Habari zinasema kuwa wakuu wa mikoa kwa nafasi zao za kuwa wenyeviti
wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, wapo kwenye tetemeko
kwa sababu unyama waliofanyiwa wananchi, nao hawawezi kupona kwa sababu
kama wangewajibika ipasavyo, ukatili uliotendeka usingefanyika.