Stori: Chande Abdallah na Denis Mtima, MWANZA
KWELI dunia ina mambo! Kijana Abel Dafe 21, mkazi wa Kayenze, Mwaloni
jijini Mwanza amezua sintofahamu ya aina yake baada ya kudaiwa kufariki
dunia na maiti yake kuzikwa wiki chache zilizopita na baadaye kuonekana
akiwa hai, bali denti wa Chuo cha Biashara (CBE) Tawi la Mwanza ndiye
akidaiwa kufa.
Abel Dafe 21.
Desemba 2, mwaka huu, Abel alidaiwa kufa maji akiogelea katika Ziwa
Victoria na mwili wake kuthibitishwa na mjomba’ake, mwili ukapelekwa
Hospitali ya Rufaa ya Bugando kabla ya kusafirishwa Sengerema kwa maziko
Desemba 4.
Akizungumza na waandishi wetu juzi, mtu wa karibu wa Abel
aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel alisema baada ya kumaliza
mazishi, familia ilirudi Kayenze, Lakini yeye Desemba 17 mwaka huu
ghafla alionana na Abel akiwa mzima wa afya maeneo ya Mwaloni.
Manyama enzi za uhai wake.
Alisema alimuweka chini ya ulinzi na kumpeleka Kituo cha Polisi cha
Kayenze na kutoa taarifa kwa ndugu waliokuwa Sengerema ambao walifika na
kujionea marehemu akiwa hai!
Kituoni hapo, Abel alikataa katakata
kuwa yeye hakufa alikuwa kwenye misele yake ila alipoteza simu ndiyo
maana hakuwa na mawasiliano na nduguze.
Kaburi la Manyama.
Ndugu hawakuyaamini mwaelezo hayo, wakati mwingine walitaka
asiwakaribie maana ni mzimu, lakini wakiwa katika maswali mengi juu ya
Abel yupi aliyezikwa, walipata taarifa kituoni hapo kuwa maiti
waliyemzika Sengerema anaitwa Manyama Chimwejo na nduguze wamepatikana.
Polisi wakaitaka familia hiyo ya Abel kukaa na familia ya Manyama
kujadili hatima, kama watafukua maiti hiyo na kwenda kumzika upya Kigoma
au watamwacha hukohuko Sengerema alipozikwa awali.
Akizungumza kwa simanzi, Abel (aliyedhaniwa kufa) alisema ndugu zake wanachojua waliyemzika ndiye Abel bali amefufuka.
“Ndugu zangu hawaamini kama mimi ni mzima hivyo napata tabu sana kwa
kuwa kila mtu ananipigia simu kuniuliza. Mimi sikufa, nilikuwa nyumbani
kwangu, tatizo lilikuwa ni mawasiliano, nilipoteza simu,” alisema Abel.
Ripoti kutoka mochwari baada ya kifo cha Abel.
Kwa upande wa pili, kaka wa marehemu aliyejitokeza kudai maiti ya
mdogo wake aliyezikwa kimakosa aliyejitambulisha kwa jina la Christopher
Chimwejo alimtaja Manyama Chimwejo (20) kuwa kweli alikuwa mwanafunzi
wa Chuo cha Biashara (CBE), Tawi la Mwanza mwaka wa kwanza na alifika
kuishi naye mapema mwezi huu baada ya chuo kufungwa.
Alisema Manyama alitoweka nyumbani kwake ghafla maeneo ya Mwaloni na
baada ya hapo hakumuona tena jambo lililomfanya atoe taarifa polisi.
Hata hivyo, sakata hilo lilimalizika Desemba 21, mwaka huu katika Kituo
cha Polisi Kirumba D ambapo pande zote mbili zilikutana na kukubaliana
kuacha kaburi la marehemu Manyama liendelee kuwa Sengerema licha ya
kwamba familia hiyo haiamini kama mwanafunzi huyo alifariki dunia.
“Hapa kuna kitu, sisi hatujafiwa na ndugu yetu, tumechezewa. Kama
ndugu yenu aliyekufa amerudi hata ndugu yetu pia atarudi tu, ngojeni
kwanza tukatambike kwetu Kigoma,” alisema kaka huyo wa marehemu.