Stori: Oscar Ndauka na Richard Manyota
NI kweli
hakuna marefu yasiyokuwa na ncha? Kama ni kweli, basi ile jeuri ya fedha
ya Miss Tanzania mwaka 2006 ambaye pia hufanya vyema kwenye gemu la
sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu inadaiwa imefikia nchani, Risasi
Mchanganyiko limepashwa ‘ei tu zedi’.
Baadhi ya magari anayomiliki Wema.
Kwa mujibu wa chanzo makini, hali ya kifedha ya staa huyo si nzuri
kiasi kwamba kwa sasa amekuwa mtu wa kushinda ndani kwa kuwa hana mpunga
unaomuwezesha kwenda kujirusha kama zamani.
SABABU NI NINI HASA?
Chanzo kilidai kwamba, binadamu aliyekuwa akimmwagia manoti staa huyo
aliyetajwa kwa jina moja la Clement ambaye ni mwajiriwa wa Ikulu jijini
Dar, yu hoi kwa kipato baada ya kunyofolewa kwenye kitengo kilichokuwa
na uwezeshaji mwingi wa fedha.
Wema akiwa ofisini kwake.
Inadaiwa kuwa, baada ya Clement ambaye ni mume wa mtu, kuondolewa
kwenye kitengo hicho amepelekwa sehemu nyingine ambayo mchana kutwa ni
kupiga miayo mpaka muda wa kutoka kazini.
MKONO WA MKEWE WATAJWA
Katika madai hayo, inasemekana mke wa Clement (jina tunalo) ana mkono
wa kile kilichompata mumewe, kuondolewa kwenye kitengo chenye ulaji na
pia amekuwa akiwawinda wawili hao ili awafanyie fumanizi kwa sababu
Clement ni mumewe wa ndoa.
Wema akiwa ndani ya nyumba aliyodai yake.
KILICHOTOKEA SASA
Chanzo kikaendelea: “Baada ya
kuondolewa kwenye sehemu yenye fedha na kutupwa kwenye ukame, jamaa
akaanza kupata tabu kwani fedha alizokuwa akimpa Wema zamani zikawa
hazipo.
“Hilo likamwathiri na Wema mwenyewe kwani ile jeuri
mliyokuwa mnamuona nayo akiifanya kwa rungu la fedha, mara sherehe, mara
kumlipia Kajala (Masanja) makahamani (Kisutu), mara kwenda baa na
wapambe imekatika ghafla.
“Siku hizi Wema ndani na yeye, yeye na ndani. Naamini hata mkienda kwake muda huu (juzi Jumatatu saa 5 asubuhi) mtamkuta.”
INADAIWA AMEUZA MAGARI MAWILI
Habari zaidi kutoka chanzo hicho, hali ilipozidi kubana sana, Wema
aliamua kuuza magari mawili kati ya matatu anayomiliki ili apate fedha
za kuendelea kujikimu katika maisha ya kila siku.
Magari hayo mawili yanasemekana ni Toyota Mark II GX 110 na Toyota Harrier na kubakiwa na Audi Q7.
YALIYOMPATA CLEMENT
Habari zinazidi kudai kwamba hali ikazidi kuwa mbaya kwa Clement kiasi
kwamba alijikuta akikabwa koo na benki moja ya jijini Dar es Salaam
ambayo aliiomba mkopo wa Shilingi mil. 120 akitumia hati ya nyumba
ambayo pia si yake.
Benki hiyo ilipozidi kumbana, mkewe (sasa wametengana) ambaye naye
anadaiwa kuwa ‘mzuri’ kwenye fedha alikwenda kulipa fedha hizo benki ili
nyumba ya watu isinadiwe na benki hiyo iliyokuwa haitaki mambo ya utani
kwenye marejesho.
Madai mengine ambayo hayajathibitishwa yanasema
kuwa, mtikisiko huo wa kifedha kwa Clement umesababisha awe ‘choka
mbaya’ kiasi cha sasa kuanza kupiga mizinga kwa rafiki zake.
WEMA ASAKWA ASEME UKWELI WAKE
Baada ya kupokea ishu hiyo, Risasi Mchanganyiko liliamua kumsaka Wema ili aseme lolote kuhusiana na tuhuma hizo.
Saa 4:32 Wema alipigiwa simu yake ya mkononi ambayo iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa hata pale iliporudiwa tena na tena.
Baada ya jitihada hizo kugonga mwamba, gazeti hili liliamua kumwendea
hewani meneja wake Martin Kadinda ambaye naye hakupokea simu licha ya
kupigiwa zaidi ya mara tatu.
Risasi Mchanganyiko halikukata tamaa, kwani ni haki ya msingi kwa
Wema kuongelea suala hilo. Likampigia msaidizi wake wa karibu anayeitwa
Pat Man, yeye alipokea, akaulizwa kuhusu bosi wake huyo, akasema:
“Wema anaumwa (hakutaja ugonjwa), ametoka hospitali sasa hivi (hakusema hospitali gani) yuko nyumbani.”
Mapaparazi wetu wakafunga safari kutoka Bamaga – Mwenge, Dar yalipo
Makao Makuu ya Nyumba ya Magazeti Pendwa Bongo, Global Publishers hadi
nyumbani kwa Wema - Makumbusho (lakini ni Kijitonyama).
Getini alikutwa mlinzi mahiri kwa mwonekano ambapo alipoombwa kumwita
Wema au kumwambia kuna waandishi wa Global wapo nje, alisema:
“Mh! Kwa kweli si rahisi kutoka, amelala anaumwa... alikwenda hospitali amerudi muda si mrefu.”
Alipochombezwa kwa maneno ya ‘kisiasa’ kwamba awaambie wasaidizi wake
wa ndani wakamwamshe, alikataa akisema litazuka timbwili ambalo yeye
hakuwa tayari kuliona.
“Bosi akilala huwa hapendi kuamshwa, hasa kama hayuko sawa. Watu wanaomwamsha ni wale wenye ahadi naye,” alisema mlinzi huyo.
WEMA ATUMIWA MESEJI
Baada ya kuondoka nyumbani kwa Wema, Risasi Mchanganyiko lilimtumia
ujumbe mfupi (SMS) ‘mreeefu’ wenye madai yote na ikaonesha ‘delivered’
kwenye simu ya Wema, lakini pia haikujibiwa.
TUNARUDI KWA CLEMENT
Simu yake haikuwa ikipatikana hewani alipopigiwa ili na yeye apewe nafasi ya kusema lolote kuhusu sakata hilo.
MKE WA CLEMENT AVUNJA UKIMYA
Risasi Mchanganyiko liliamua kumsaka kwa simu ya mkononi mke wa Clement
ambapo alipopokea na kusomewa mashitaka ya mumewe na nafasi yake kama
shahidi muhimu alikiri hali ya jamaa kuwa tete kimfuko.
“Kuhusu hilo
la nyumba ni kweli ilikuwa inadaiwa na benki (aliitaja jina) na
walitaka kuinadi ili wapate fedha zao, lakini nikaingilia kati ili
kulinda heshima ya familia.
“Unajua ile nyumba kuna mtu alituuzia, kwa hiyo Clement alitoa kiasi
cha fedha lakini hakumalizia na akatumia hati ya nyumba kwenda kuombea
huo mkopo. Kwa sababu benki walikuja juu nilitafuta mtu akainunua, kiasi
cha fedha nikammalizia aliyetuuzia na kulipa benki,” alisema mwanamke
huyo.
KUHUSU KUMFANYIA FITINA MUME AKAHAMISHWA KITENGO
Huyu hapa mke wa Clement: “Hilo si kweli bwana. Kwanza mimi ndiyo
nilimfikisha pale alipofika. Sasa mtu nimuinue mwenyewe nitamfanyiaje
fitina?
“Kwanza mimi siko naye siku hizi. Nilipoona anachukua magari
ya nyumbani na kuyapeleka huko kwa nani sijui (Wema) nikaamua kukaa
pembeni na kunyamaza kimya.
“Kama ni mabalaa anayapata hukohuko aliko, nisisingiziwe mimi kwa lolote lile.”
KUHUSU KUMWANDALIA FUMANIZI WEMA
“Aaa wapi!
Nimwandalie fumanizi la nini? Yeye ana maisha yake mengine mimi niko na
mambo yangu, muda huo sina kabisa, yaani niko bize sana,” alisema
mwanamke huyo huku akidai muda huo alikuwa akidraivu.
PRODYUZA WA WEMA ALIJUA HILI?
Wiki mbili zilizopita, gazeti damu moja na hili, Ijumaa Wikienda
liliandika katika ukurasa wake wa mbele habari yenye kichwa; MAGARI YA
WEMA YAGEUZWA GESTI.
Katika habari hiyo, Wema alidaiwa kumtimua kazi
prodyuza wake katika Kampuni ya Endless Fame, Rashid Mohammed ‘Chid
Classic’ kwa sababu ya kumtuhumu kufanya ufuska kwenye magari yake
maeneo ya Ufukwe wa Coco, Dar.
Siku chache mbele, prodyuza huyo
alifunguka katika gazeti lingine pendwa ndani ya mjengo, Amani kuwa,
Wema ‘amechoka’ siku hizi, halipi mishahara wafanyakazi wake na alitaka
yeye awe kuwadi ndiyo wangeendana jambo ambalo yeye hakuwa tayari. .
HABARI NYINGINE YA MJINI
Yapo madai kuwa,
kutokana na maswahibu hayo ya kuwa kwenye wakati mgumu kifedha, kampuni
yake imeanza kudoda na mbaya zaidi, marafiki zake anaokuwa nao kwenye
raha, wamemkacha na kumwacha akihangaika mwenyewe.
“Msiniandike
gazetini lakini ukweli ni kuwa, huu ndiyo wakati wake wa kujifunza
kuchagua marafiki. Ona sasa, wale wote aliokuwa akila nao raha, wamekaa
pembeni. Ni tatizo sawa, lakini pia ni funzo kwa upande mwingine,”
alisema mpambe mmoja anayefanya naye kazi kwa karibu sana.