Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro ogin’g
MKE wa marehemu bilionea Suleiman Muhema, Zihija Muhema ametoboa siri
kuhusiana na kifo cha mume wake aliyekutwa amefariki dunia kwa kujipiga
risasi akiwa ndani ya gari lake Kisarawe, Pwani.
Mke wa marehemu bilionea Suleiman Muhema, Zihija Muhema.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Zihija alisema kifo cha mume wake
kimegubikwa na usiri mkubwa baada ya mumewe siku ya tukio kumwambia kuwa
anamfuata mama yake aliko, hali ambayo ilimshitua kwa kuwa mama yake
mzazi alishafariki siku nyingi zilizopita.
“Mume wangu alikuwa na siri kubwa kwani baada ya kifo chake nimeamini kuwa kuna mambo mengi alifanya bila kunishirikisha.
Bilionea Suleiman Muhema enzi za uhai wake.
“Hadi anakufa nilikuwa sijui kama anamiliki bastola, hali ambayo
imenipa imani kuwa huenda chanzo cha kujiua alikuwa anakijua,” alisema.
Aliongeza kuwa siku ya tukio mume wake alimpigia simu na kumwambia
ikifika saa 4.30 usiku ampigie simu na wakati huo ilikuwa ni saa 2.
Akasema kuwa alimjibu kuwa atakuwa amelala lakini alimsisitizia afanye hivyo na baadaye alisema anakwenda kujiua.
“Ilipofika saa nne usiku nilimpigia na kumuliza yuko wapi, aliniambia
yupo kati ya Minaki na Kisarawe anakwenda kujiua hali ambayo ilinipa
wasiwasi mkubwa.
Gari alilokuwa nalo marehemu Suleiman.
“Nilipomuuliza kwa nini anataka kufanya hivyo? Aliniambia maelezo yote atayaacha polisi.
“Tuliendelea kuongea na mume wangu ili aniambie yuko wapi ili niweze kumfuata lakini akanijibu kuwa anamfuata mama yake alipo.
“Nilimuliza kama ni kujiua kwa nini aende mbali akajibu kuwa anaweza
kuchukua maamuzi ya kujiua halafu asife hivyo anaona ni heri awe mbali
na hospitali ili iwe kazi kupona kama ataenda kuokolewa.
“Nilimuliza
tena sababu ya kujiua, alikata simu. lakini kabla ya hayo yote
nilimuuliza akifa tukamzike wapi? Akajibu Dar karibu na watoto wake,”
alisema mke huyo.
Uchunguzi wa gazeti umebaini kuwa marehemu aliwahi kulalamikiwa na
mkewe huyo Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar kuwa alimtishia maisha na
likafunguliwa jalada lenye kumbukumbu namba OB/RB/12734/2013, Julai 20
mwaka huu.
Hata hivyo, jalada hilo lilifungwa Agosti 5, mwaka huu baada ya wanandoa hao kuelewana.
Mke wa marehemu alipoulizwa kuhusu hilo alikiri na kusema katika ndoa mambo kama hayo yapo na waliyamaliza.
Akizungumzia mali za marehemu, mama huyo alisema hivi sasa kuna maneno
mengi yanasemwa kuhusu magari makubwa, akasema yapo na hayajapotea
ambapo ni Scania namba T 793 CHE, T 159 CGF na T 331 CHK ambayo
aliyanunua yeye (mke) lakini alimkabidhi mumewe kusimamia.
“Ninasikitika kusikia kuna watu wanaosema vibaya, kama ni ndugu wa marehemu wafike kuniona kwa ajili ya kuwekana wazi,” alisema