AWALI
ya yote, nianze kwa kumshukuru sana Mungu wa mbinguni kwa jinsi
anavyoendelea kutenda miujiza katika maisha yetu. Kila kinachotutokea ni
kwa sababu yake na hakuna lolote ambalo tunaweza kumlaumu zaidi ya
kumshukuru kwa vile kila jambo linakuja kwa sababu maalum.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Baada ya angalizo hilo, naomba sasa nije moja kwa moja kwenye mada
yetu ya leo. Miezi michache iliyopita, tunakumbuka kwamba taifa
lilitangaza oparesheni maalum ya kutokomeza ujangili, ikiwa na lengo la
kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote waliokuwa
wakijihusisha na uwindaji haramu, kiasi cha kuhatarisha uwepo wa
wanyama, hasa tembo na faru.
Ni oparesheni kubwa iliyolenga siyo tu kuwaokoa wanyama na kukomesha
vitendo hivyo vya ukiukwaji wa sheria, bali pia ilikuwa na nia ya
kutokomeza kabisa mtandao huo, unaodaiwa kuwa mkubwa, ndani na nje ya
nchi.
Katika utekelezaji wake, serikali iliamua kutumia nguvu kubwa,
kwa kuyaingiza katika oparesheni hiyo majeshi yetu (Polisi na JWTZ),
viongozi wa kaya zinazoishi karibu na maeneo ya hifadhi, askari wa
wanyama pori na watu wengine wote ambao waliaminika kwa njia moja au
nyingine, watasaidia kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Lakini katika hali ya kusikitisha, vijana hawa wanaolipwa mishahara
kwa kodi za wananchi, waligeuka na kuharibu maana nzima ya zoezi hilo,
kiasi cha kusababisha uharibifu mkubwa wa mali, udhalilishaji wa hali ya
juu pamoja na dhuluma kwa watu.
Badala ya kuwasaka majangili na
kuwatokomeza, watu waliingia katika vijiji na kuvichoma moto bila sababu
za msingi, kuwabaka akina mama, kuwapora fedha, mifugo na wakati
mwingine kusababisha mauaji kwa watu wasiokuwa na hatia.
Ulikuwa ni unyama wa hali ya juu ambao Watanzania waliwafanyia
Watanzania wenzao katika namna ambayo inasikitisha sana. Wananchi
kupitia kwa wawakilishi wao bungeni walilalamikia zoezi hilo na kwa
kauli moja, bunge likaridhia kusimamishwa kwa oparesheni hiyo, ili
kulipa nafasi ya kufanya uchunguzi na kuja na majibu.
Kamati ya bunge
iliyoundwa kuchunguza tukio hilo, iligundua kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa
wa maadili na haki za binadamu, hali iliyowafanya mawaziri watatu
kutakiwa kuachia ngazi na mmoja kutangaza kujiuzulu muda mchache kabla
ya waziri mkuu kutoa tangazo hilo la kuwasimamisha bungeni.
Huu ni uamuzi ambao ulipaswa kuchukuliwa hasa ukiangalia unyama
waliofanyiwa watu ambao hawakuwa walengwa. Lakini wakati hali imetokea
hivi mawaziri hawa, ambao wamewajibishwa kwa kitendo cha kutowasimamia
vizuri walio chini yao, nadhani sasa lazima upande wa pili wa shilingi
uangaliwe, uchunguzwe na hatua zichukuliwe.
Hawa waliohusika katika kuwabaka mama na dada zetu, waliojichukulia
sheria mikononi na kupora mifugo ya wafugaji, kuchoma moto nyumba na
vyakula vya wananchi, kuwatesa, kuwadhalilkisha na hata kuwasababishia
vilema vya kudumu na vifo, ni lazima washughulikiwe kisheria.
Tutakuwa hatutendi haki kwa Watanzania kama tutawaacha watu hawa
waendelee na maisha yao wakati wamefanya ukatili mkubwa kwa wananchi.
Kwa sababu wanafahamika ni lazima wafikishwe mahakamani kwa mashtaka
wanayostahili ili haki itendeke.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli!