Kocha wa zamani wa Yanga, Ernie Brandts.
Uongozi wa klabu ya Young Africans SC umempatia taarifa (Notice) ya
siku ya thelathini (30) kocha mkuu mholanzi Ernie Brandts juu ya
kusitisha mkataba wake kuanzia jana Disemba 22 mwaka huu.
Maamuzi hayo yanafuatia muenendo wa matokeo mabaya katika michezo
iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya
Simba SC mwishoni mwa wiki.
Hatua ya Young Africans SC kusitisha huduma na Brandts isichukuliwe
kama chuki bali ni moja ya sehemu ya kuhakikisha tunaboresha benchi la
ufundi ili tuweze kupata matokeo mazuri katika Mashindano
yanayotukabili.
Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga SC na wapinzani
wetu, na soka tulilocheza kwenye mchezo wa mwishoni mwa wiki kwa kweli
ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.
Young Africans SC imekua ikicheza chini ya kiwango katika michezo ya
Ligi Kuu hali iliyoplekea kupata ushindi kwa tabu na wakati mwingine
timu kupoteza pointi.
Kufuatia kupewa taarifa ya siku 30, Brandts ataamua mwenyewe kama
ataendelea kusimamia mazoezi ya timu au kuondoka moja kwa moja kabla ya
muda huo ukiwa haujakamilika.
Ikiwa Brandts ataondoka mapema
timu itaendelea na mazoezi kama kawaida katika kila siku asubuhi katika
uwanja wa bora kijitonyama kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na
mashindano ya kimataifa chini ya kocha msaidizi Fred Felix “Minziro”.
Ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu ya Vodacom na mashindano ya kimataifa uongozi unakamilisha
maandalizi ya safari ya kambi nje ya nchi na taratibu zote
zitakapokamilika tutawajulisha.
Aidha uongozi upo katika
mchakato wa kumapata mrithi wa Brandts ambaye ataungana na timu kwa
ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili na Mashindano ya klabu Bingwa
Afrika.
Mwisho tunawaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa
Yanga wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza mwishoni mwa wiki,
uongozi unajipanga kuhakikisha timu inaimarika kwenye benchi la ufundi
na kurudisha furaha katika mzunguko wa pili wa VPL.
Abdallah Bin Kleb
Mwenyekiti - Kamati ya Mashindano
Young Africans Sports Club.
DAR ES SALAAM
23 Disemba, 2013