Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakabidhi rasimu ya pili ya Katiba kwa
Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein,
Desemba 30, mwaka huu.
Makabidhiano hayo yatafanyika katika hafla itakayofanyika katika
Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam baada ya Tume kumaliza kazi yake ya
kuiandaa.
Rasimu hiyo ya pili inatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume
hiyo ilipotoa rasimu ya kwanza ya ambayo ilijadiliwa katika Mabaraza ya
Katiba yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 20 (2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mara
baada ya Rais kukabidhiwa rasimu hiyo, itachapishwa katika Gazeti la
Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.
Pia katika
kipindi hicho, Rais anatakiwa kuitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba
kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa. Kutokana na hali hiyo,
kuna uwezekano mkubwa kuwa Bunge la Katiba litaanza vikao vyake
Februari, 2013.
Taarifa ya Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid
iliyotolewa jana ilieleza kuwa Tume hiyo itakabidhi rasimu hiyo kwa
Marais Kikwete na Dk Shein katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na
wananchi wa kawaida.
Tume hiyo ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa
rasimu ya pili Desemba 15 mwaka huu lakini Rais Kikwete aliiongezea
siku 14 zaidi hadi Desemba 30, mwaka huu.
Hatua hiyo ya Rais
Kikwete kuiongezea muda tume hiyo ilikuwa ya pili. Mara ya kwanza
iliomba kuongezewa muda wa siku 45, kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba
15, mwaka huu. Kabla ya kuomba kuongezewa muda mara ya kwanza, ilitakiwa
kukamilisha kazi yake Novemba 30.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
inaelekeza Tume hiyo kufanya kazi kwa miezi 18 licha ya kuwa inampa
Rais mamlaka ya kuiongezea muda usiozidi siku 60.
Hatua ya Rais
kuiongezea muda kwa mara ya pili, ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa
wajumbe wake kujipanga upya baada ya kifo cha mwenzao, Dk Sengondo
Mvungi kilichotokea Novemba 12, mwaka huu huko Afrika Kusini alikokuwa
akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotolewa Juni 4, mwaka huu.