Muigizaji wa filamu Aunt Ezekiel Grayson amevunja ukimya na kupinga
vikali tetesi za ujauzito wake kuhusishwa na mmoja wa mawaziri wa sasa
wa maliasili na utalii akibainisha kuwa jambo hilo linautesa moyo wake.
Akizungumza na GPL, Aunt alifunguka kwamba, mbali na kumzushia juu ya
ujauzito huo, kuwa mara ya kwanza watu asiowajua walieneza uvumi kuwa
alikwenda nchini Marekani na mheshimiwa huyo lakini aliwapuuza kwa kuwa
alikwenda kwa kazi yake ya sanaa.
“Kuna binadamu hawajali maumivu ya mtu mwingine, inawezekanaje mtu
aanze kuropoka kitu kizito kama hicho tena mtu na familia yake, sasa mtu
ambaye ndiye muhusika wa ujauzito huu anajisikiaje?
“Ukweli mimba yangu siyo ya waziri, ifahamike kuwa namheshimu sana
mheshimiwa, najisikia vibaya mtu anapoeneza kitu cha namna hiyo,”
alisema Aunt kwa uchungu mkubwa.
Aunt alitiririka kwamba, mbali na uvumi huo, pia alishangazwa na
baadhi ya wabunge waliothubutu kuzungumza kuhusu yeye na waziri huyo
tena bungeni kwenye kujadili vitu vya msingi badala yake wanazungumza
mambo ambayo hayana kichwa wala miguu.
“Hivi inawezekana kweli kabisa wabunge ambao tunawaheshimu wanakwenda kuzungumza vitu vya ajabu bungeni?
“Wamenifanya nisiwe naangalia hata hilo bunge kabisa,” alisema Aunt.
Staa huyo alimalizia kuwa mambo hayo yanampa wakati mgumu na kumuumiza
kwa sababu madai yanayozungumzwa ni mazito huku yakiwa hayana chembe ya
ukweli zaidi ya kuleta mfarakano kwenye familia ya waziri huyo ambaye
pia ni mbunge.
Mbali na waziri huyo, pia Aunt alikanusha kuwa mimba kubwa aliyonayo
si ya yule mcheza shoo wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond’, Mose Iyobo
kama wengi wanavyodai.
Kuhusu hilo, GPL lilizungumza na Mose Iyobo ambaye alisema kuwa
anachojua ujauzito ni wa kwake lakini akashangazwa na uzushi usiokuwa na
kichwa wala miguu.
Swali ni je , kama Aunt anamruka Mose Iyobo na amekasirishwa na
tetesi za kuhusishwa na waziri huyo ambaye ni mume wa mtu huku mumewe,
Sunday Demonte akidaiwa kufungwa Dubai, je, mimba hiyo ni ya nani?