Mashabiki wa timu ya Yanga Fc.
WATANI wa jadi katika soka nchini, timu za
Yanga na Simba, leo zinashuka katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam kuhitimisha majigambo ya ‘Nani Mtani Jembe’ baina yao katika
mechi kali inayofanyika chini ya uratibu wa mdhamini wao, Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL).
Mashabiki wa timu ya Simba Fc.
Mbali ya wapenzi na mashabiki wa timu hizo kusubiri kuona ‘nani mtani
jembe’ kati yao, pia watapata fursa ya kushuhudia nyota wapya
waliosajiliwa kupitia dirisha dogo.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema maandalizi ya mechi hiyo ya
aina yake yamekamilika.
Wambura alisema vikosi vya ulinzi na
usalama katika mechi ya leo vimekamilika kila idara na kwamba Barabara
ya Taifa inayoanzia Keko-Maghorofani hadi Barabara ya Mandela, itafungwa
kuanzia saa 12 asubuhi kupisha hekaheka za mtifuano huo.
Alisema magari hayataruhusiwa kuegeshwa kuanzia eneo la Baa ya Minazini
hadi msikiti unaotazamana na Uwanja wa Uhuru, hivyo magari yote
yataegeshwa nje ya Uwanja wa Ndani wa Taifa – kando ya Barabara ya
Mandela.
“Magari yatakayoruhusiwa kuingia maeneo hayo na hata
ndani ya Uwanja wa Taifa ni yatakayokuwa na stika zilizotolewa na TFF.
Tunawaomba wadau na mashabiki wa soka kuheshimu na kutii maagizo ya
vikosi vya ulinzi,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa milango ya
kuingilia uwanjani itakuwa wazi kuanzia saa sita mchana ambapo baada ya
mauzo ya tiketi ya jana, zoezi hilo litaendelea leo nje ya uwanja huo
kabla ya mechi ili kuwapa mashabiki fursa ya kukata na kuingia moja kwa
moja.
Pambano la leo linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka
wanaohitaji sio tu kuona nyota wapya waliosajiliwa na klabu hizo, pia
kujua ‘nani jembe’ ndani ya uwanja kwani kwa nje ya uwanja, Yanga ni
kama imeshinda kutokana na kuwa kwenye mazingira mazuri kisaikolojia.
Nje ya uwanja, Nani Mtani Jembe ilihusisha vita baina ya mashabiki wa
kila klabu ‘kupora’ mamilioni ya mwingine kupitia shindano la kinywaji
cha Kilimanjaro Premium Lager ambapo Simba ilizidiwa na Yanga kwa kiasi
kikubwa cha pesa.
Ukiondoa shangwe ya mashabiki wa Yanga
kumpata mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi akitokea SC
Villa ya Uganda na Juma Kaseja, Simba leo itakuwa na makipa waliowahi
kudaka Jangwani kwa vipindi tofauti, Ivo Mapunda na Yaw Berko.
Nyuma ya majina hayo makubwa, Yanga ilinasa saini ya kiungo Hassan
Dilunga kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, wakati Simba iliwasainisha kwa
mpigo kiungo mchezeshaji Awadh Juma Issa kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro
na Ally Badru Ally kutoka Canal Suez ya Misri.
Kila timu
ilishajichimbia kambini kunoa makucha kuelekea pambano hilo ili
kusawazisha makosa yaliyowafanya watani hao kutoka sare ya 3-3 katika
mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Oktoba 20.
Uwepo wa nyota wapya kwa kila upande ambao watashirikiana na wakali
wengine, unalifanya pambano la leo liwe lenye mvuto wa aina yake ambapo
kiingilio cha chini ni sh 5,000 kwa viti vya kijani.
Kwa upande
wa viti vya rangi ya bluu, kiingilio ni sh 7,000; viti vya rangi ya
chungwa sh 10,000; VIP C ni sh 15,000; VIP B sh 20,000 huku VIP A sh
40,000.
Kwa upande wa waamuzi, kati atasimama Ramadhan Ibada
‘Kibo’ wa Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na
Simon Charles wa Dodoma huku Israel Nkongo wa Dar es Salaam akiwa
mezani. Kazi ya kutathimini utendaji wa waamuzi wote itakuwa chini ya
Soud Abdi wa Arusha.
MECHI TANGU 2010
Rekodi ya watani
hawa inaonyesha kuwa mechi ya leo ni ya tisa tangu mwaka 2010 na katika
mechi nane, Yanga imeshinda tatu, Simba mbili na wamekwenda sare tatu.
Aprili 18, 2010: Simba 4, Yanga 3
Oktoba 16, 2010: Yanga 1, Simba 0
Machi 5, 2011: Yanga 1, Simba 1
Oktoba 29, 2011: Yanga 1, Simba 0
Mei 6, 2012: Simba 5, Yanga 0
Oktoba 3, 2012: Yanga 1, Simba 1
Mei 18, 2013: Yanga 2, Simba 0
Oktoba 20, 2013: Simba 3, Yanga 3