SERIKALI mkoani Kagera imewataka wahamiaji haramu waliorudi tena nchini huku wakijiita M23 na kuteka kijiji cha Kibingo kilichoko wilayani Kyerwa huku wakiendelea kutoa vitisho kwa wananchi kuondoka mara moja kwani wakikamatwa watafikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa kosa la ujambazi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabiani Masawe alipofanya ziara wilayani humo na kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Benedict Kitenga kutoa taarifa juu ya hali halisi ya maendeleo ya zoezi la Operesheni Kimbunga awamu ya nne katika eneo lake.
“Nimepata taarifa kutoka kwa wananchi wa wilaya hii kuwa wahamiaji haramu wamerudi kwa nguvu na wanawatisha wananchi kwa kuwaeleza kuwa watawaua. Serikali haitavumilia watu hao wakaendelea kuwatisha wananchi. “Naagiza Kamati za Ulinzi na Usalama hususani Usalama wa Taifa kufanya uchunguzi na kuweka mtandao ambao utawapa taarifa zitakazowawezesha kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahamiaji haramu hao kwa kosa la ujambazi. Kwakweli hatuwezi kuwaita wahamiaji haramu bali hawa ni majambazi,” alisema Massawe.
Alisema kiongozi yeyote kuanzia ngazi ya kata mpaka mkoa atakayeonekana kuwakingia kifua wahamiaji hao kwa kuchukua fedha na mifugo yao kwa lengo la kuendelea kuwaficha na kuwarudisha hapa nchini atashitakiwa kwa kosa la usaliti wa Taifa huku akiwataka wananchi kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapowaona watu hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Luten Kanali mstaafu Benedict Kitenga alisema Serikali ya Wilaya kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama walipata taarifa kwamba wahamiaji haramu wamerudi kwa kasi katika Kijiji cha Kibingo na kuteka eneo la kijiji hicho huku wakijiita M23 wakiwa na silaha za jadi ambazo ni mikuki, mapanga, visu na marungu wakitishia wananchi na watendaji wa maeneo hayo kuwa wakiwasema watawajeruhi.
“Tulienda mpaka kijijini hapo na tulipofika katika eneo walilokuwa wamejimilikisha tulifanikiwa kukuta wahamiaji haramu zaidi 2,018 kutoka nchi za Uganda na Rwanda ambapo walikuwa katika harakati za kukutafuta chakula hapo kijijini wakiwa na silaha hizo za kijadi wakitishia wananchi wakiwataka wawape vyakula kwa nguvu ila tulifanikiwa kuwakamata wote na kuwarudisha makwao na kuwanyang’anya silaha.”
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, George Mikindo alisema kuwa viongozi wa maeneo hayo ndio wanaowalea wahamiaji haramu hao, na kuleta shida ya kuwajua kwani hawatoi ushirikiano kwa sababu wamekuwa wakiwafuata wahamiaji hao haramu Rwanda na kuwarudisha nchini ili wawachungie mifugo.