SERIKALI imefanya mabadiliko ya sheria ya ushuru wa bidhaa kwenye kadi za simu iliyokuwa ikitaka kulipa Sh 1,000 kwa mwezi kwa kila kadi na sasa kila mtumiaji wa huduma za mawasiliano kulipa ushuru unaolingana na matumizi yake.
Pia imepandisha kiwango cha ushuru wa huduma za mawasiliano kutoka asilimia 14.5 hadi asilimia 17 ambapo itaanza kulipwa kuanzia Januari mwakani.
Hatua hiyo imefuatia Rais Jakaya Kikwete kutokusaini muswada huo wa sheria hivyo kusababisha kuletwa tena bungeni kwa hati ya dharura ambapo wabunge wote waliipitisha huku wakitaka kuangalia viwango hivyo kwenda sambamba na nchi za Afrika Mashariki.
Awali akiwasilisha marekebisho hayo, Kaimu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema katika marekebisho hayo serikali itakusanya Sh bilioni 148 huku Sh bilioni 30 zitalipwa na makampuni ya simu ili kukamilisha makadirio ya mapato ya ushuru wa huduma za mawasiliano katika mwaka wa fedha 2013/14, fedha ambazo zinakusudiwa kukamilisha mafungu ya bajeti iliyopitishwa ya maji na umeme vijijini.
Alisema serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwa kufuta ushuru huo ili kufidia pengo la mapato litokanalo na hatua hiyo kwa kupandisha kiwango cha ushuru huo wa huduma za mawasiliano kutoka asilimia 14.5 hadi asilimia 17.