Stori: Oscar Ndauka na Ojuku Abraham
DUNIA ipo kimya wakati maandalizi ya kuupumzisha kaburini mwili wa aliyekuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela yakiendelea katika miji ya Johannesburg, Pretoria na kijijini Qunu, Mkoa wa Mthatha jimboni Eastern Cape atakozikwa kijijini atakakozikwa.
UKIMYA WATANDA KWENYE TELEVISHENI
Ukimya uliendelea kutawala juzi na jana katika miji mbalimbali duniani, watu walikusanyika kwenye televisheni za wazi kufuatilia zoezi la kuuaga mwili huo zilizofanyika katika Jengo la Umoja jijini Pretoria.
Maelfu ya waombolezaji walionesha kuguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huo unaotajwa kushika rekondi tangu kuwepo kwa ulimwengu kuwahi kutazamwa na watu wengi zaidi kuliko mingine yote iliyowahi kutokea.
Mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Romani Katoliki Duniani, Papa John Paul wa II unatajwa kushika rekodi ya kwanza hadi Desemba 5 mwaka huu alipokufa Mandela.
PICHA ZA TELEVISHENI ZATAWALIWA NA VIDEO ZA MANDELA
Vituo vingi vya televisheni sehemu mbalimbali ulimwenguni, licha ya kuonesha tukio hilo la kuaga mwili, pia viliweka video ya matukio mbalimbali yaliyowahi kufanywa na kiongozi huyo anayetajwa kama mwanamapinduzi wa kweli, mpigania haki na mwanaharakati aliyeheshimika kuliko mwingine katika karne ya 21.
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na jinsi alivyoshiriki shughuli mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na kupiga picha na wanamichezo, wasanii wengi maarufu, ambao pia walionesha kufurahishwa naye kila alipokutana nao.
SERIKALI SAUZI YASAMBAZA SETI YA TELEVISHENI NCHI NZIMA
Serikali ya Afrika Kusini imesambaza seti ya televisheni zipatazo 90 nchi nzima na kuwekwa katika maeneo mengi ya wazi kwa lengo la kuwawezesha mamilioni ya wananchi wake kuangalia shughuli za kumuaga kiongozi huyo zinavyokwenda.
KIJIJINI QUNU KAMA MJINI
Katika Kijiji cha Qunu alichokulia hayati Mandela, maandalizi ya kaburi atakalozikwa yapo tayari huku kijiji hicho kikijaa watu na kuwa na maisha kama mjini.
Magari ya kila aina yanaingia na kutoka, watu wasiofanana na maisha ya kijijini wanapatikana kwa sasa, wengi wao wakiwa wageni, wakiwemo wa vyombo vya habari, wanaingia na bidhaa zao, hususan chakula.
NDEGE YA KIJESHI KUMPELEKA MANDELA KIJIJINI KWAKE
Serikali ya nchi hiyo imetamka kuwa, mwili wa hayati Mandela utapelekwa kijijini Qunu kwa ndege ya jeshi la nchi hiyo, tayari kwa mazishi yake Jumapili ya Deseamba 15.
WAZEE WA KIMILA WATOA MSIMAMO KUHUSU MAZISHI
Taarifa kutoka kijijini hapo zinasema kuwa jamii ya Kabila la AbaThembu (ndivyo inavyaondikwa), imetaka kukabidhiwa shughuli za mazishi hayo ili shujaa huyo aweze kuzikwa kwa mujibu wa mila za kabila lake.
Kiongozi wa jamii ya Xhosa (lugha ya Waaba Thembu), Nokuzola Mndende alisema kuwa endapo serikali itapuuza matakwa yao ipo hatari ya Mandela kutopokelewa na miungu hivyo roho yake kurejea duniani na kuisumbua familia yake.
“Zitakuwa ni mila na desturi za jadi, serikali inapaswa kutupa nafasi na isituingilie. Ng’ombe dume (fahali) atachinjwa kwa ajili ya kumsindikiza marehemu kaburini,” alisema kiongozi huyo bila kupindisha maneno kinywani.
Aliongeza: “Katika utaratibu huu wa mazishi ya kimila ni familia ya Mandela pekee ndiyo watakaohusika kumwandalia safari njema Madiba.”
Kwa mujibu wa desturi za mazishi za kabila hilo, mtu aliyefariki dunia endapo alikuwa kiongozi, hupewa heshima ya kuchinjiwa ng’ombe dume ili amsindikize ambapo damu yake hunyunyiziwa juu ya kaburi.
TARATIBU ZA MAZISHI ZA KIKABILA
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, zipo taratibu maalum ambazo ni lazima zifuatwe wakati wa mazishi ya mtu wa kabila moja na mzee Mandela.
Baada ya mtu kufariki dunia, ni jukumu la wanafamilia ya marehemu kutangaza msiba huo kwa ndugu na jamaa ili waweze kukutana na kusaidiana wakati wa mazishi.
Kabla ya ujio wa vyumba vya kisasa vya kuhifadhia maiti (mochwari), Waaba Thembu walikuwa wakimzika mtu siku hiyohiyo kwa kuhofia mwili wake kuharibika.
Kabla ya kufanyika kwa mazishi, taratibu zinasema vyombo vyote vilivyomo ndani ya nyumba hutolewa nje na wanawake wanaohusiana na marehemu ni lazima wafanye usafi katika nyumba aliyokuwa akiishi.
Katika siku za nyuma, kuta za kibanda kikubwa kilichokuwa kikitumiwa na marehemu kulala kilikandikwa udongo, lakini hivi sasa nyumba kubwa kwa kawaida husafishwa na kupakwa rangi upya.
Baada ya usafi huo, mkeka wa kiasili huwekwa katika chumba kikubwa cha kulala ambako mjane wa marehemu hutakiwa kukalia mkeka huo unaowekwa chini ya dirisha.
Uchaguzi wa ng’ombe mnono wa kiume hutegemea na umuhimu wa marehemu na wanaume ndiyo wanaopika nyama hiyo katika vyungu vya kikabila ikichemshwa bila kuwekwa kiungo chochote.
Tukio hili huitwa Umkhapho inayodaiwa kuwa ni mizimu ya kumsindikiza mtu aliyefariki dunia.