
Zitto Kabwe akihutubia wananchi wa Kigoma jana.
Wananchi wakiwa na mabango ya kumpokea Zitto.
HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013
Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye
changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si
salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu,
uzalendo na uwajibikaji. Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu
wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania;
kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna
nafasi ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za
kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza.
Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi
mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya
mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo mlitoa
madiwani wengi mwaka 1994.
Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu
kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma
hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi
zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika
nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika
mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu
haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika
kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si
maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na
maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule
ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu
yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma.
Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na
kwenye siasa kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa
darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa
vinatengenezwa na Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha
Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama
Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la
hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili
kwenda la tatu.
Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na
hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji kwani
alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa
kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii
hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii
kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili
katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa
kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya
juu sana.
Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka
niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia.
Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya
kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha
mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na
miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa
kukosa ajira na kukuza umasikini.
Demokrasia inahusu maendeleo. Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa
mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo
mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo
ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara
za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa
kituo cha Usafirishaji Mwandiga.
Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi
watu wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu
bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi
wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya
uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima
ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma
katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea
maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa
makuu.
Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi
cha utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka
kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa
Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna
watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini
watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na
sio Kigoma tu.
Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye
sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo
yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na
hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya
asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani.
Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa
ya Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii
ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia
ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo
wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri
Mkuu.
Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni
taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za
Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa
kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na
ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika
kuimarisha demokrasia yetu.
Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana. Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa
kwa kiasi kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila
Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi
wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe
kwa wenyewe.
Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni uongo.
Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya na
ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli. Kukosekana
kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu. Itachukua
muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama
hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa
ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa
badala ya kutafutwa.
Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza
shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na
Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema
sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo. Ni
uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo
ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne.
Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na
taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki
wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria. Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja
majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu
utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi
kama mtu binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia
dosari harakati hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika.
Sitaingia mtego huu! Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea
kujiuliza maswali mengi kwa mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo
gani? Na ninajikuta hata mimi ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya
KUTOAMINIANA.
Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi
sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za
kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga
vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za
mawazo na uhuru wa mawazo.
Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na
tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa
woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi
unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na
kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima vyama vya siasa,
viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa
yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu.
Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni
vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule.
Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio
kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na
hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo
sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa
inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya
kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa.
Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti
ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo!
Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia
umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi.
Ninasukuwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila
ninapoona akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona
vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa
kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua
chai asubuhi.
Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika
hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na
utoroshwaji wa pesa zetu. Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti
ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee,
jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi
trilioni 2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini
Tanzania. Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani
shilingi za kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni
1.3) zilitoroshwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa
nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani
milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni
7,286,860,000,000 (trilioni 7.3). Nimewatajia hapa namba chungu nzima
na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba
kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake
tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka
Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa
vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata
huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu.
Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu
ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi
zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya
viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia
macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia
ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa
kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!
Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za
kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea
bila sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika
mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana
mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na
ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili
kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra
zake zinakuwa huru.
Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki
kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna
maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko
huleta matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi
hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya
kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha;
ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo.
Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa
zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo
wananchi wa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.