SHINYANGA, Tanzania
DIWANI
wa Kata ya Nyida wilayani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM), Shindiko Masele(40) amekufa papo hapo baada ya kupinduka na
pikipiki aliyokuwa akiendesha.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Sosteness Ngassa alisema diwani huyo
alipata ajali hiyo jumamosi saa 2.30 usiku wakati alipojaribu kumkwepa
mwendesha baiskeli na kusababisha pikipiki yake kupoteza mwelekeo na
ikagonga mti uliokuwa kando ya barabara.
Ngassa alisema baada ya pikipiki hiyo kugonga mti diwani huyo
alianguka chini na kufa papo hapo huku abiria aliyekuwa amebebwa
aliyetambuliwa kwa jina la Silasi Ngoni alijeruhiwa kidogo kwa kupata
michubuko ambapo hata hivyo alikimbizwa katika hospitali ya serikali
mkoani Shinyanga alikotibiwa na kuruhusiwa.
Makamu mwenyekiti
huyo alisema kifo hcho kilichotokea ghafla kimewasikitisha na kwamba
halmashauri yake imepoteza mmoja wa viongozi muhimu na ameacha pengo
ambalo halitokuwa kuwa rahisi kuzibika kwa siku za hivi karibuni.
Alisema hivi sasa wanaendelea na maandalizi ya shughuli za mazishi
ambapo mwili wa marehemu ulikuwa umehifadhiwa katika hospitali ya
serikali mkoani Shinyanga na kwamba iwapo mipango itakwenda kama
ilivyopangwa mazishi yake yalitarajiwa kufanyika leo mchana kijijini
kwake Nyida.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga,
Annarose Nyamubi alisema amepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo
cha diwani huyo na kwamba alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa mstari wa
mbele katika suala zima la uhimizaji wa maendeleo katika kata yake na
usimamiaji wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.
“Nimeshitushwa na taarifa za kifo cha diwani wetu wa kata ya Nyida, kwa
kweli inasikitisha sana, maana ametutoka ghafla, ameacha pengo ndani ya
halmashauri yetu na katika kata yake, alikuwa mstari wa mbele katika
suala zima la uhimizaji wa maendeleo katika eneo lake ni wazi
tutamkumbuka daima,” alisema Nyamubi.
Marehemu Masele
alizaliwa mwaka 1973 wilayani Shinyanga na ameacha mjane mmoja na watoto
watatu a ambapo wakati akipata ajali hiyo alikuwa akitokea Kata ya
Isaka wilayani Kahama akirejea kijijini kwake Nyida.