Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
NI
jambo lililotoa mshtuko kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kisarawe, mkoani
Pwani ambapo Desemba 10, mwaka huu, walikuta mwili wa binadamu ukiwa
ndani ya gari lililopinduka, pembeni mwa Barabara ya Kisarawe -
Mwaneromango.
Mbali na mwili, ndani ya gari hilo aina ya Toyota RAV 4 (milango mitatu
new model) lenye namba za usajili T 273 AKP kulikutwa bastola moja,
risasi 85 na magazini mbili.
Utata ukaanzia hapo, polisi wa wilaya hiyo wakiongozwa na mkuu wao
(aliomba jina lisitiriwe kwa sababu si msemaji) wakajiuliza ni nani mtu
huyo ambaye alikuwa amefariki dunia? Kumbe alikuwa Suleiman Muhema (42),
bilionea kijana mkazi wa jijini Dar es Salaam.
polisi waliuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Wilaya mpaka ndugu walipokwenda kuuchukua kwa mazishi.
SULEIMAN MUHEMA NI NANI?
Suleiman Muhema ni mkazi wa jijini Dar, amejenga jumba la kifahari Kijitonyama ambako aliishi na mke wake, Zihji Mvungi (42).
Mpaka kifo chake alikuwa mfanyabiashara wa magari kutoka Japan akiyauza
Dar, pia alikuwa na kampuni ya usafirishaji, sifa zote kwa pamoja
zinamfanya aitwe bilionea.
MAISHA SIKU CHACHE KABLA YA KIFO
Habari zinadai kuwa, marehemu alikuwa ndani ya mgogoro wa kifedha na mtu ambaye hakutajwa jina lakini ni wa karibu naye.
Inadaiwa kuwa, mgogoro huo ni wa muda mrefu na ulikuwa ukisuluhishwa na Dawati la Jinsia, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar.
SIKU YA TUKIO
Siku
ya tukio inadaiwa marehemu alikuwa Magomeni na watu (idadi yao
haikujulikana). Baada ya hapo aliondoka kwenda kusikojulikana lakini
baadaye alimpigia simu ndugu wa karibu na kumwambia kuwa yuko mahali
(hakupataja) ametekwa na sauti anayoitoa inaweza kuwa ya mwisho kisha
akakata simu.
MAELEZO YA POLISI SASA
Kwa
mujibu wa chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Kisarawe,
Desemba 10, mwaka huu, usiku wa saa nane, marehemu alionekana akiwa
ndani ya gari jeusi umbali wa kilomita saba kutoka Kisarawe Mjini lakini
aliondoka baada ya kuliona gari la ‘patroo’ ya polisi.
Chanzo hicho kikasema kuwa dakika chache mbele polisi waliokuwa katika
shughuli za ulinzi usiku huo waliliona gari hilo likienda pembezoni mwa
barabara na kupinduka.
“Tulilifuatilia, tukalikuta limepinduka, ndani ya gari tulimkuta mtu
amekufa kwa kujipiga risasi kwani sehemu ya kidevuni na kwenye utosi
kulikuwa na tundu la risasi,” kilisema chanzo hicho.
MAREHEMU ALIDHANIWA MHALIFU
Habari
zinasema katika upekuzi wa awali ambapo polisi walimkuta marehemu akiwa
na bastola, risasi 85 na magazini mbili walidhani alikuwa mhalifu
aliyetaka kutekeleza uhalifu mahali ndani ya walaya hiyo.
NDUGU WA MAREHEMU WANA NENO
Kwa
upande wao ndugu wa marehemu ambao waliomba majina yao yawekwe pembeni,
walisema kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu kifo cha ndugu yao huyo kwa
sababu hata kifo chake hawakielewielewi.
Akizungumza kwa hisia ya
uchungu, ndugu mmoja alisema katika maisha ya jijini Dar, yeye ndiye
baba wa marehemu lakini hakuna alichojua toka kifo hadi kuzikwa.
Alisema hata mazishi ya marehemu alishtukizwa kwamba anazikwa siku hiyo jambo lililompa wakati mgumu kufikiria.
“Sisi
kama ndugu wa marehemu, tulipenda akazikwe nyumbani, Makete (Njombe),
lakini ghafla tukaambiwa anazikwa hapahapa Dar tena siku hiyohiyo
tuliyopewa taarifa,” alisema ndugu huyo.
MKE WA MAREHEMU NAYE
Kwa
upande wake mke wa marehemu Zihji alipoulizwa na mapaparazi wetu juzi
kuhusu sakata la kifo cha mumewe alijibu kuwa kila mtu anaweza kuongea
jambo lolote.
Aliongeza kusema anachojua yeye ni kwamba kifo cha mumewe kilitokea kama ambavyo mtu mwingine angeweza kufa.
KAMANDA WA POLISI ANASEMAJE?
Kamanda
wa Polisi mkoani Pwani, ACP Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kusema kuwa marehemu alikutwa akiwa na jeraha la risasi
moja hali ambayo ilionesha alijipiga risasi mwenyewe pengine kutokana na
mambo yaliyokuwa yakimsonga kichwani.
BILIONEA AZIKWA DAR
Marehemu
Muhema alizikwa Desemba 11, mwaka huu kwenye Makaburi ya Sinza jijini
Dar. Ameacha mke na watoto watatu wa kike. Mungu ailaze pema peponi roho
yake. Amina.
MASWALI TATA
Kifo cha Muhema kina maswali tata mengi. Kwanza, kama kweli alipanga kujiua kwanini alikwenda mbali na Jiji la Dar es Salaam?
Pili, kwa nini damu ndani ya gari ilikuwa kidogo wakati uzoefu unaonesha
kuwa, mtu anayepigwa risasi ndani ya gari huacha damu nyingi?
Tatu, ndugu mmoja wa marehemu alikiri kuwa, Muhema alinunua bastola
mwaka huu ili kujilinda, sawa kabisa. Je, kwa nini akutwe na risasi
nyingi kiasi hicho kama alikuwa anakwenda kufanya uhalifu?
Nne, ilidaiwa alimpigia simu ndugu mmoja akidai ametekwa na huenda
asisikike tena. Polisi walikuta simu kwenye gari lake, kwa nini waseme
alijipiga risasi mwenyewe