Mafanikio
maishani yana sura nyingi. Tunatofautiana katika maana nzima ya
mafanikio.Unachokiona wewe kuwa ni cha mafanikio yawezekana jirani yako
akakiona si mali kitu.
Pamoja na tofauti
hizo za maana au matinki ya mafanikio,wengi tunakubaliana kwamba furaha
na amani maishani ni miongoni mwa mafanikio au malengo muhimu sana ya
binadamu. Kila mtu anataka kuishi maisha yaliyojaa furaha na amani.Ndio
maana tunapokumbwa na vitu ambavyo kibinadamu havikaribii kabisa maana
ya furaha na Amani,wengi wetu huangua vilio,kujuta,kulaumiana,kufarakana
nk.Kila mtu anatamani kutokuwa na huzuni au masononeko mbalimbali
moyoni.
Tunatofautiana
pia katika mbinu za kujenga maisha yenye furaha na amani. Kwa
wengine,kuwa na pesa nyingi ndio furaha.Ndio kipimo chao cha furaha.Kwa
mwingine kuendesha gari ya thamani kubwa ndio kipimo cha furaha
yake.Mifano ipo mingi.
Pamoja na tofauti
za kimantiki na mbinu za kuwa na furaha na amani,yapo mambo mbalimbali
madogo madogo(kwa wengine yanaweza kuwa makubwa) ambayo binadamu anaweza
kuyafanya ili kujiongezea furaha maishani na kuwa na amani zaidi.Haya
ni mambo ambayo sote tunaweza kuyafanya bila kuzingatia sana jinsia wala
hali za vipato vyetu. Ni mambo gani hayo? Leo tutaangalia baadhi ya
mambo hayo.
-
Piga marufuku mawazo hasi(negative thoughts):
Furaha ya kweli huanzia kwenye akili yako na mawazo yako. Ukijipa
mawazo hasi,ni wazi kwamba kitu kinachoitwa furaha utakuwa unakipiga
kikumbo kwenda nje.
Bahati nzuri ni
kwamba kama binadamu,tumepewa uwezo mkubwa wa kuchagua. Unaweza kuchagua
kuilisha akili yako mawazo hasi,yasiyojenga,yasiyo leta maendeleo
yoyote au unaweza kuamua kuilisha akili yako mawazo chanya(positive
thoughts),ya kimaendeleo na yanayojenga.Chaguo ni lako.
Nimeshawahi
kusikia watu mbalimbali wakilalamika kwamba hawana furaha maishani. Cha
ajabu ni kwamba watu hao hao ukiwasikiliza sana katika maongezi
yao,wamejaa mawazo hasi.Kila kitu kwao ni kibaya,kila mtu ni mbaya.
Mahali pa kuanzia ni kichwani,akilini mwako.Jijengee tabia ya kuhifadhi
mawazo mazuri. Mabaya achana nayo.Hayakufai na huna muda nayo.
-
Angalia mazuri ya kila jambo:
Hili halitofautiani sana na hilo hapo juu. Tofauti inakuja katika
utekelezaji. Wakati kupiga marufuku mawazo hasi kunatokea au kunatakiwa
kutokea kabla ya tukio au matukio fulani, hili la kuangalia mazuri
katika kila jambo hutokea baada ya kitu fulani. Kwa mfano:Una mtoto
ambaye hakusikilizi? Badala ya kuzidi kumfokea na kulaani bahati yako ya
kumzaa,kwanini usitumie nafasi hiyo kumfundisha jinsi na faida ya
maelewano miongoni mwa binadamu. Kwanini usichukulie hali hiyo kama
mojawapo tu ya mambo ambayo wewe kama mzazi ni lazima uyapitie? Kwanini
usimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa mtoto kwani unajua kabisa kwamba
wapo wengine wengi ambao wanaomba kupata mtoto/watoto?
Ushauri wangu ni
kwamba angalia mazuri ya kila jambo. Unapokabiliwa na majaribu ambayo
yangeweza kukudidimiza katika mawazo hasi,chagua upande mzuri.Jiulize
naweza kujifunza nini kutokana na jambo hili? Je kuna lolote zuri?
-
Fanya mazoezi:
Naelewa kwamba sio kila mtu ni mshabiki au mpenzi wa mazoezi.
Nimeshawahi kuongea na binti mmoja ambaye alidiriki kabisa kuniambia
kwamba yeye hakuumbwa afanye mazoezi. Anasema mazoezi sio sehemu ya
maisha yake na wala haitokaa iwe.
Kwa ufupi binti
yule anakosea. Hajazingatia analolisema na kuliamini.Naomba nikuambie
kitu kimoja; tabia ya kufanya mazoezi inaweza kukuletea muujiza wa
furaha maishani mwako.Ingawa watu wengi hufanya mazoezi kwa nia ya
kuboresha muonekano wao, mazoezi ni njia nzuri sana ya kuondoa mawazo
mabaya,maradhi mbalimbali ambayo husababisha ukosefu wa furaha na amani.
Mazoezi huleta
dhana ya kujiamini na pia ni njia nzuri ya kupata marafiki wapya
maishani. Anza taratibu tu.Unaweza kuanza kwa kufanya mazoezi japo kwa
dakika kumi tu kwa siku. Tembea badala ya kupanda gari,kimbia, nenda
gym,cheza muziki nk.Sina shaka kabisa kwamba utaona jinsi gani maisha
yako yatabadilika. Kama tayari wewe ni mtu wa mazoezi,usiache hata
kidogo.Endelea.
-
Chukua likizo/mapumziko:
Pamoja na juhudi zote za kuyafurahia maisha hakuna jambo jema maishani
kama mapumziko.Miili na akili zetu za kibinadamu hufikia mahali
vikachoka. Unapojipa muda wa kupumzika unajipa nafasi ya kujipatia nguvu
mpya,mawazo mapya.
Labda hii naweza
kuifananisha na kauli mbiu ya kampeni iliyopita ya uraisi ambayo ilikuwa
ni kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya. Kila inapowezekana pata muda wa
mapumziko.Pata muda wa kuachana na ratiba yako ya kawaida.Kama wewe ni
mkulima basi hebu jaribu kuachana na kilimo japo kwa mwezi
mmoja.Pumzisha mwili,pumzisha akili.
-
Jitolee/Saidia wenzako:
Utamaduni wa kujitolea bado hauna umaarufu mkubwa hapa nchini kwetu
ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea. Hali duni za kiuchumi,
zinasababisha watu wengi wasifanye shughuli za kujitolea kwa kisingizio
cha ukosefu wa muda,ukosefu wa vitendea kazi nk.
Lakini hakuna
jambo ambalo linaleta furaha ya kweli maishani kama kufanya shughuli za
kujitolea(volunteer) au kumsaidia mtu mwingine katika jambo lolote lile.
Ni kweli kwamba wengi wetu tuna hali duni. Ni kweli kwamba muda kwa
wengine inaweza kuwa tatizo. Lakini jiulize,ni muda kiasi gani unautumia
pale baa kwenye kiti kirefu au pale kibarazani ukipiga soga na rafiki
zako? Unaonaje kama muda huo ungeutumia kwenye shughuli za kujitolea?
Badala ya kushinda kijiweni, kwanini usijiunge na wenzako mkaenda
kumsaidia mzee mmoja asiyejiweza kufanya usafi wa mazingira ya nyumbani
kwake?
Kujitolea na
kusaidia wengine sio tu msingi wa kujenga jamii iliyo bora bali pia ni
njia muhimu ya kuleta furaha na amani maishani mwako. Anza
leo,jitolee/saidia wengine. Tumia ujuzi,afya njema na uwezo wowote
uliopewa na Mungu kusaidia wenzako na kusaidia jamii yako.
Kumbuka kwamba
orodha ya mambo ya kufanya yaweza kuwa ndefu zaidi. Chochote kile
unachoweza kukifanya bila kumbughudhi mwenzako au wanajamii wenzako na
ukaona kinakuletea furaha na amani maishani mwako, nakushauri uendelee
kukifanya.Hivyo ndivyo utakavyoweza kufanya ili kujiongezea furaha na
amani maishani mwako na pia kuwaongezea wengine furaha na amani.
Title : MAMBO MATANO(5) YANAYOWEZA KUKUFANYA UWE NA FURAHA NA AMANI.
Description :
Rating : 5